Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ameungana na mfadhili maarufu duniani, Bill Gates, katika hafla ya Goalkeepers iliyofanyika usiku kuamkia leo jijini New York, Marekani.
Hafla hiyo, iliyoandaliwa na Taasisi ya Bill & Melinda Gates Foundation, ilikusanya viongozi, wadau wa maendeleo na watu mashuhuri kutoka pande mbalimbali za dunia, wote wakiwa na lengo la kuhamasisha uwekezaji katika afya na maendeleo endelevu.
Mada kuu ya mwaka huu ilikuwa ni afya ya watoto chini ya miaka mitano, ambapo wadau walijadiliana namna ya kuhakikisha vizazi vijavyo vinakua salama, vyenye afya njema na kupata huduma bora za msingi.
Dkt. Kikwete, ambaye kwa muda mrefu amekuwa kinara katika masuala ya afya na elimu barani Afrika, alibadilishana mawazo na Bill Gates juu ya mbinu bora za kuwekeza katika afya, hususan katika kuimarisha upatikanaji wa chanjo, huduma za mama na mtoto, na elimu kwa jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Kikwete alisisitiza kuwa maendeleo ya taifa lolote yanategemea afya njema ya wananchi wake, hasa watoto, ambao ndio nguvu kazi ya kesho. Alisisitiza umuhimu wa kuwekeza zaidi katika huduma za afya za msingi ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030.
Kwa upande wake, Bill Gates alibainisha kuwa ushirikiano wa kimataifa na uwekezaji wa pamoja katika sekta ya afya ndio silaha kubwa ya kuondoa vifo vya watoto vinavyoweza kuzuilika, na kusisitiza kuwa dunia inapaswa kushirikiana ili kufanikisha lengo hilo.
Hafla ya Goalkeepers imekuwa jukwaa la kimataifa linalowakutanisha viongozi, wabunifu na wanasiasa, likilenga kushirikisha uzoefu na mipango ya harakati za kufanikisha malengo ya maendeleo endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDGs).