Dar es Salaam – Wazee na Wenyeviti wa Matawi wa Klabu ya Yanga leo Juni 5, 2025 wamejitokeza hadharani makao makuu ya Klabu hiyo na kutoa tamko rasmi wakipinga vikali ushiriki wa klabu hiyo katika mchezo wa watani wa jadi (derby) uliopangwa kufanyika tarehe 15 Juni, 2025 Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Kupitia kikao maalum kilichofanyika jijini Dar es Salaam, wazee hao wamewaomba mashabiki na wanachama wa Yanga, hususan walioko mikoani, kutojisumbua kufika Dar kwa ajili ya mchezo huo, wakisisitiza kuwa klabu haina mchezo wowote katika tarehe hiyo.
“Tunawaomba mashabiki wetu wa mikoani wabaki majumbani. Hakuna sababu ya kujitokeza kwa ajili ya mchezo ambao haupo kwenye ratiba ya klabu,” alisema mmoja wa wazee hao kwa niaba ya wenzake.
Aidha, wazee hao wamevitaka vyombo vya habari nchini kutoitaja Yanga kwenye matangazo au kampeni yoyote inayohusiana na mchezo huo wa Juni 15, wakisisitiza kuwa klabu haitahusishwa kwa namna yoyote.
“Vyombo vya habari visitupotoshe mashabiki. Kama kuna mchezo unatangazwa, Yanga haitakuwa sehemu yake. Hatutaki jina la Yanga litumike kwenye matangazo yasiyo rasmi,” aliongeza.
Katika hatua nyingine, wazee hao wamewaonya vikali viongozi wa klabu hiyo dhidi ya kuchukua maamuzi ya kupeleka timu uwanjani siku ya mchezo. Wameeleza kuwa iwapo hilo litatokea, wao kama wazee hawatakuwa na budi kuchukua hatua kali, ikiwemo kujiondoa au kutotambua uamuzi huo.
“Hatutakubali klabu iongozwe kwa maamuzi ya ghafla bila kuzingatia maslahi ya Yanga. Kama timu itaenda uwanjani, basi wajue njia ni nyeupe kwa sisi wazee kuachia ngazi,” walisema kwa msisitizo.
Tamko hili linakuja wakati kukiwa na sintofahamu kuhusu hatima ya mchezo huo wa jadi, huku kukiwa na mvutano wa chini kwa chini kuhusu maandalizi na uhalali wake kwani Klabu ya Yanga inadai kuwa Simba walisusia mchezo Machi 8, 2025.
Mpaka sasa Bodi ya Ligi haijatoa maamuzi yoyote kuhusiana na tukio hilo.