WANACHOKITAKA SIMBA KIMATAIFA HIKI HAPA, KAZI IPO

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa ambacho wanahitaji kwenye mchezo wao wa hatua ya nusu fainali dhidi ya Stellenbosch FC ya Afrika Kusini ni ushindi mkubwa ambao utawapa tiketi ya kufuzu hatua ya fainali moja kwa moja kwenye dakika 90 za mwanzo.

Timu hiyo chini ya benchi la ufundi linaloongozwa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, nusu fainali yake ya kwanza inatarajiwa kuchezwa Jumapili ya Aprili 20 2025, Uwanja wa New Amaan Complex na ile ya pili ya kuamua mshindi atakayetinga fainali itachezwa Afrika Kusini.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa kazi ambayo wanayo kwa sasa ni moja kupambana kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wao wakiwa nyumbani, Jumapili.

“Jumapili tuna kazi ya kumnyoa Stellenbosch. Tunahitaji kupata ushindi mkubwa, yaani sisi kufuzu fainali tunaipata hapa hapa Uwanja wa Amaan. Tumalizane naye mapema hapa na tunachotaka mwaka huu ni kwenda fainali. Dalili zote zinaonyesha huu ni mwaka wa mafanikio wa Simba Sports Club. Timu yetu ipo vizuri na palipobaki ni padogo kwa sisi mashabiki kuiunga mkono.

“Huyu ni mpinzani wa kawaida tena tunamzidi ubora. Tumeshafika nusu fainali na hii haiishia hapa tunaitaka fainali. Tunataka kushinda ubingwa wa Afrika, tunataka kuendelea kuheshima Afrika, tunataka kuendelea kupata ubora wa Afrika. Sababu nyingine ya kutaka kwenda fainali ni kuwaumiza watu moyo. Kuna watu wanaumia, kuna watu wanateseka, na sisi wakiumia tunaendelea kukandamiza ili waumie na ili kuumia ni Mnyama kwenda fainali.

“Furaha yetu ni kuona wanaendelea kuumia. Njia pekee ya kumuumiza mtu mwenye roho mbaya ni wewe kufanikiwa. Wanasimba tusikubali kuishia nusu fainali. Ndugu zangu safari hii mwisho wake ni fainali. Hili jambo tunaliweza sana, hili jambo lipo ndani ya uwezo wetu. Tukishikana Mnyama anakwenda fainali. Wazanzibari wakiamua lao linawezekana, twendeni uwanjani Jumapili tuionyeshe duania. Hakuna sababu ya kubaki nyumbani tarehe 20, wewe mwenyewe anza kujionea aibu kama ukishindwa.

“Tunaitaka fainali. Hakuna mwaka mzuri wa mafanikio kama huu, kila kitu kinatuendea vizuri. Twendeni tukaimalize hii, twendeni tukachukue ubingwa. Kwani inashindikana nini? Timu tunayo ya kufanya hivyo. Mwaka huu hatuhitaji kingine chochote zaidi ya Simba kwenda fainali ya Kombe la Shirikisho. Kwa ufupi tunataka ubingwa wa kombe la Shirikisho Afrika na hilo linawezekana.

“Jina la Simba Sports Club liliasisiwa na Hayati Abeid Amani Karume hivyo Simba ilianzishwa na Wazanzibari. Maana yake Simba na Zanzibar ni damdam, na hii haiwezi kuwa kazi ngumu kwa Wazanzibari kuipeleka Simba fainali. Fainali inapatikana kwa michezo miwili lakini sisi tunataka kuimaliza hapa hapa Zanzibar. Tunataka kupata ushindi mkubwa, ushindi mnono ili Mnyama awe kwenye nafasi ya kwenda fainali.”