KUELEKEA kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya KMC dhidi ya Yanga unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC, Complex benchi la ufundi la Yanga limebainisha kuwa hesabu kubwa ni kupata pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo unaotarajiwa kuchezwa Februari 14 2025.
Kocha Mkuu wa Yanga Miloud Hamdi amesema kuwa wamejeandaa kiakili ili kuhakikisha kwamba wanapata ushindi kwenye mchezo huo na kuwapa furaha mashabiki wa timu hiyo baada ya kuvuna pointi moja kwenye mchezo uliopita.
“Tumejiandaa kiakili kuhakikisha tunapata ushindi na kuepuka kuwavunja moyo mashabiki wetu. Sisi sote, benchi la ufundi na wachezaji tunatamani sana kushinda mchezo wa kesho.
“Ninakubaliana na mashabiki wana kila sababu ya kutoridhika kwa sababu sisi ni klabu kubwa na mashabiki wanataka kushinda kila mchezo. Amini, hata sisi makocha na wachezaji tunataka kushinda kila mchezo. Kwa hiyo, kesho tutafanya kila tuwezalo kushinda mchezo huu kwa sababu tunahitaji alama tatu.
“Ninataka kuwapa ujumbe mashabiki wa Yanga kwamba tunapambana na kufanya kazi kwa bidii kwa ajili yao na wachezaji wanajua wanachopaswa kufanya kesho na pia katika siku zijazo. Tuko hapa kushinda mataji, hatuko hapa kwa ajili ya kazi tu, mashabiki wetu wasikate tamaa kwa sababu ya sare moja bado tuna michezo mingi ya kucheza. Kila kitu kinawezekana, bado hatujachelewa, tuna muda, lakini lazima tufanye kila tuwezalo kushinda michezo yote ili kuwapa furaha mashabiki wetu kwa sababu wao wako pamoja nasi, na sisi pia tuko pamoja nao.”
Kwenye msimamo Yanga ipo nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 18 ambazo ni dakika 1,620 ikiwa imekusanya jumla ya pointi 46 kinara ni Simba mwenye pointi 47.