TFF YAMFUNGIA MIAKA MITANO MWENYEKITI WA KAMATI YA UCHAGUZI YA CHAMA CHA DRFA

Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imemfungia miaka mitano kujihusisha na mpira wa miguu Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salam (DRFA), Yusuph Kaiwanga.

Katika uamuzi wake, Kamati imesema baada ya kupitia ushahidi wa nyaraka na maelezo ya shahidi imejiridhisha pasi na shaka kuwa Mlalamikiwa Kaiwanga alitenda makosa kwa makusudi.

Kamati ilijiridhisha kuwa Mlalamikiwa hakutumia vyema mamlaka aliyopewa kisheria kusimamia uchaguzi wa Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Temeke (TEFA) na kuamua kuufuta.

Hatua yake ya kuufuta haikuwa sahihi kwa vile alishiriki mchakato mzima wa uchaguzi huo. Hivyo, Kamati ya Maadili imeamua matokeo ya uchaguzi wa TEFA yanabaki kama yalivyo.

Mbali ya kifungo cha miaka mitano, Kamati pia imemtoza Mialamikiwa faini ya sh. milioni sita. Adhabu hizo zimetolewa chini ya kifungu cha 73(4) na (5) cha Kanuni za Maadili za TFF, Toleo la 2021.

Awali Kaiwanga alilalamikiwa mbele Kamati ya Maadili kuwa kitendo chake cha kufuta Uchaguzi wa TEFA wakati alishiriki mchakato mzima tangu mwanzo kilikiuka Kanuni za Maadili za TFF.