KOCHA MPYA YANGA ATAJA NGUZO MUHIMU

IKIWA ni mchezo wake wa kwanza kimataifa akiwa kwenye benchi la ufundi la Yanga, Kocha Mkuu, Sead Ramovic amesema kuwa hakuna staa ndani ya timu hiyo huku nguzo zake kuu anazosimamia ikiwa ni nidhamu na kujituma kwa wachezaji wake.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa saa 10:00 jioni ambapo mashabiki wameitwa kujitokeza kwa wingi uwanjani kushuhudia mchezo huo wa kimataifa.

Novemba 26 2024 ni Dube Day ambapo Yanga yenye mastaa kadhaa ikiwa ni pamoja na Clatous Chama, Djigui Diarra, Clement Mzize, Pacome, Dickson Job, Aziz Ki, itakuwa na kibarua cha kusaka pointi tatu dhidi ya Al Hilal ya Sudan ukiwa ni mchezo wa hatua ya makundi.

Kocha huyo amebainisha kwamba ni furaha kwake kuwa ndani ya Yanga ambayo ni timu kubwa anaamini watafanya vizuri kwenye mechi ambazo watacheza licha ya kwamba unakuwa ni mchezo wake wa kwanza.Ikumbukwe kwamba kocha huyo amerithi mikoba ya Miguel Gamondi ambaye alifutwa kazi kutokana na mwendo wat imu hiyo kuwa wa kusuasua.

Kocha huyo amesema: “Yanga ni timu bora sana, lakini tunakwenda kucheza na timu bora pia hivyo tunahitajika tuwe makini sana. Tunapaswa kuwa na utayari kiakili na kisaikolojia kwani tunakwenda kwenye mechi ngumu. Hata hivyo ninayo furaha kubwa kuiongoza klabu kubwa kwenye mashindano makubwa.

“Hii ni mara yangu ya kwanza kwenye ligi ya mabingwa. Ni jambo la kheri sana kwangu kushiriki mashindano haya makubwa nikiwa na timu kubwa ya Yanga. Falsafa yangu kubwa ni nidhamu na kujituma. Napenda kuona wachezaji wakicheza kama timu, haijalishi unatumia mfumo gani kama wachezaji wako hawana umoja ni ngumu kupata matokeo

“Kwenye timu yangu sina mchezaji mashuhuri (Staa) kuliko mwingine. Wachezaji wote nawapa haki sawa kwa kuzingatia juhudi zao kwenye uwanja wa mazoezi. Ili tushinde lazima wachezaji wawe na umoja. Natambua ubora wa kila mchezaji lakini jambo la muhimu kwangu ni namna gani mchezaji anatumia uwezo wake kuipa timu matokeo.”

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.