KUELEKEA kwenye mchezo wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa Simba dhidi ya Bravos mgeni rasmi wa mchezo huo ni pasua kichwa kuwa hayupo kwenye orodha ya wachezaji yeye ni Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally.
Simba chini ya Kocha Mkuu, Fadlu Davids ipo kwenye maandalizi ya mwisho kwa ajili ya mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa ikiwa ni hatua ya makundi hivyo msako wa pointi tatu kila mchezo unaendelea kwa sasa.
Ahmed amesema: “Tarehe 27 tuna jambo kubwa kwenye Uwanja wa Mkapa. Tunahitaji kuanza vizuri hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ushindi wa Simba unakutegemea wewe Mwanasimba, tambua ya kwamba tiketi utakayonunua ni silaha muhimu ya kuisaidia Simba siku hiyo.
“Tunatambua siku hiyo ni siku ya uchaguzi wa Serikali za mitaa, ukishamaliza kupiga kura yako elekea Uwanja wa Mkapa. Asibaki Mwanasimba siku hiyo, tambua kwamba ushindi wa Simba unapatikana kwa ushirikiano wa nguvu wa kila Mwanasimba.
“Tumejiandaa siku hiyo kila Mwanasimba atakayekuja uwanjani aondoke na furaha. Tumedhamiria msimu huu kila anayekuja lazima tumfunge. Kwahiyo ndugu zangu Wanasimba jukumu letu la msingi ni kwenda uwanjani na ukienda uwanjani usitulie, unafanya balaa unaloweza.
“Mgeni rasmi katika mchezo wetu dhidi ya Bravos atakuwa ni Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally Mgeni rasmi ni mimi hapa.”