HONGERA TAIFA STARS, YAFUZU AFCON 2025

KUTOKA kundi H, timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inayonolewa na Kocha Mkuu, Hemed Morocco imekata tiketi kufuzu AFCON 2025 kwa ushindi dhidi ya Guinea.

Baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Mkapa umesoma Tanzania 1-0 Guinea ambapo katika dakika za lala salama Guinea walikuwa wanatafuta pointi moja kwa kutaka kumtungua Air Manula ambaye alianza kikosi cha kwanza.

Bao la ushindi katika mchezo wa leo limefungwa na Simon Msuva dakika ya 62 na alionyeshwa kadi ya njano baada ya kushangilia kwa kuvua jezi.

Ni Mudathir Yahya alitoa pasi iliyomkuta Msuva akiwa ndani ya 18 na kumtungua Mousa Camara ikumbukwe kwamba Msuva alikosa nafasi tatu kwenye mchezo wa leo akiwa ndani ya 18 jambo lililofanya ashangilie kwa furaha alipofunga bao.

Pointi 10 Stars inafikisha ikiwa nafasi ya pili huku nafasi ya kwanza ikiwa ni DR Congo yenye pointi 12, Guinea nafasi ya tatu na pointi 9 huku Ethiopia ikiwa nafasi ya nne ikiwa na pointi moja.

Hongera Taifa Stars, hongera mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Mkapa.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.