SIMBA QUEENS WAITULIZA YANGA PRINCESS

KWENYE ulimwengu wa soka la Wanawake Tanzania ushindani unazidi kuwa mkubwa kila iitwapo leo ambapo mchezo mkali wa Kariakoo Dabi uliochezwa Uwanja wa KMC, Mwenge ni Simba Queens waliibuka wababe.

Baada ya dakika 90 kwenye mchezo huo ubao ulisoma Yanga Princess 0-1 Simba Queens huku bao la ushindi likifungwa na Vivian Corazone kipindi cha pili.

Ikumbukwe kwamba dakika 45 za mwanzo ngoma ilikuwa ngumu kwa timu zote kwenye kucheka na nyavu mpaka kipindi cha pili ambapo Simba ilikomba pointi tatu mazima.

Esther Mayala nyota wa Simba Queens amesema kuwa haikuwa rahisi kupata ushindi kutokana na uimara wa wapinzani wao lakini walitumia maelekezo ya benchi la ufundi kupata matokeo.

“Ilikuwa ni kazi kubwa uwanjani kwa kuwa kila timu ilikuwa inahitaji matokeo na mwisho tumepata ushindi, tulisikiliza maelekezo kutoka kwa benchi la ufundi tukafanikiwa kupata pointi tatu muhimu.”

Baada ya kucheza mechi nne msimu wa 2024/25 Simba Queens inafikisha jumla ya pointi 12 ikiwa nafasi ya kwanza imeshinda mechi zake zote ndani ya uwanja.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.