RAIS WA SHIRIKISHO LA SOKA LA AFRIKA KUSINI (SAFA) DANNY JORDAAN AKAMATWA

Rais wa Shirikisho la soka la Afrika Kusini (SAFA) Danny Jordaan amekamatwa kufuatia madai ya kutumia pesa za Shirikisho hilo kujinufaisha binafsi, kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini humo.

Jordaan, ambaye alichukua jukumu kubwa katika kuandaa Kombe la Dunia la 2010 nchini Afrika Kusini, alijaribu kuzuia kukamatwa kwake siku ya Jumanne, lakini jana alikamatwa.

Kukamatwa huko kulifuatia uvamizi wa polisi katika ofisi za SAFA mwezi Machi, ambapo msemaji wa polisi Katlego Mogale alisema kuwa”kati ya 2014 na 2018, Rais wa SAFA alitumia rasilimali za shirika hilo kujinufaisha binafsi, ikiwa ni pamoja na kuajiri Kampuni binafsi ya ulinzi kwa ajili ya ulinzi binafsi na kampuni ya mahusiano ya umma , bila idhini kutoka kwa bodi ya ya SAFA.

Jordaan (73) na watuhumiwa wenzake, Mkurugenzi wa Fedha wa SAFA Gronie Hluyo na mfanyabiashara Trevor Neethling, wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani.