BODI ya Ligi Kuu ya soka Tanzania (TPLB) imethibitisha kupokea barua ya klabu ya Yanga Sc ya kuomba kuutumia uwanja wa KMC Complex kwa michezo yake ya nyumbani badala ya Azam Complex ambako walikuwa wanautumia awali ingawa ombi hilo bado halijatolewa majibu.
Akizungumzia ombi hilo, Afisa Habari wa TPLB, Karim Boimanda amesema ombi la Yanga Sc linaangukia kwenye kanuni ya tisa ya TPLB inayotoa ruhusa kwa klabu ambayo haina uwanja wa nyumbani kuchagua uwanja mwingine ambao utakuwa ndani ya mkoa ule ule ambao walikuwa wanacheza ama mkoa wa jirani ilimradi uwe unakidhi vigezo.
“Barua ambayo Young Africans Sc wameiandikia Bodi ya Ligi inaeleza kuwa klabu hiyo haina uwanja, wameshamalizana na wamiliki wa uwanja wa Azam Complex, Chamazi kwa hiyo wanakwenda kuangukia kwenye hiyo kanuni ya 9 ibara ya 4.” —— amesema Boimanda.