YANGA YAFUNGUKIA ISHU YA DUBE KUTOFUNGA

UONGOZI wa Yanga umebainisha kuwa suala la mshambuliaji wa timu hiyo kutofunga litafika mwisho kwani licha ya kusemwa sana wapo wachezaji wengine ambao wamecheza muda mrefu bila kufunga ndani ya uwanja.

Ikumbukwe kwamba Dube aliibuka Yanga akitokea kikosi cha Azam FC ambapo huko kwenye mechi ambazo alicheza alifunga mabao 7 msimu wa 2023/24 miongoni mwa timu ambazo alizifunga ilikuwa Simba kwenye mchezo wa ligi uliokamilika kwa ubao kusoma Simba 1-1 Azam FC.

Katika mchezo huo bao la Simba lilifungwa kwa pigo la faulo na kiungo mshambuliaji Clatous Chama ambaye kwa sasa naye yupo ndani ya kikosi cha Yanga.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wanasikia kuhusu mchezaji wao Dube kutofunga jambo ambalo halina maana kubwa kwani mchezaji huyo uwezo wake unafahamika na akipata nafasi atafunga mabao mengi.

“Naskia wengi wanasema kuhusu Dube kutofunga hilo linawafanya wapige kweli makelele wakati kuna mchezaji anatimiza mwaka mmoja yaani siku 365 bila kufunga hilo wamekaa kimya hawasemi.

“Hakuna kitu kama hicho ambacho kinazungumzwa zaidi ni Dube ambaye kacheza mechi 8 bila kufunga, nimemwambia Dube aache presha akae hata miezi mitatu atulie kuna mtu kacheza mwaka hajafunga.”

Novemba 7 Yanga itakuwa na kibarua cha kusaka ushindi kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Tabora United unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.