UBUTU WA SAFU YA USHAMBULIAJI WAMLIZA KOCHA MSIMBAZI

KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu Davids ameweka wazi kuwa kuna tatizo kwenye eneo la ushambuliaji hasa katika umaliziaji wa nafasi ambazo wanatengeneza ndani ya uwanja jambo ambalo linawafanya wakose kufunga mabao mengi kwenye uwanja.

Novemba Mosi 2024 Simba ilicheza mchezo wa kwanza ikiwa ugenini ndani ya Novemba na baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Lake Tanganyika, mwisho wa reli Kigoma ulisoma Mashujaa 0-1 Simba.

Bao pekee la ushindi kwa Simba lilifungwa na mshambuliaji mrefu kuliko goli Steven Mukwala dakika ya 90 kwa pigo la kona iliyopigwa na Awesu Awesu.

Fadlu amesema kuwa walipata nafasi zaidi ya mbili kwenye mchezo huo walishindwa kuzitumia kuwa bao jambo lililowafanya wakasubiri kupata bao la dakika za lala salama.

“Ulikuwa ni mchezo mgumu na unaona kwamba tulipata nafasi zaidi ya mbili kwenye mchezo wetu na wachezaji walishindwa kuzitumia hii iliongeza ugumu wa mchezo wenyewe.

“Licha ya wapinzani wetu kufanya kazi kubwa uwanjani tunashukuru tumepata bao na pointi tatu katika dakika za mwisho hivyo tutakwenda kufanyia kazi makosa yetu.”

Simba inafikisha jumla ya pointi 22 ikiwa nafasi ya tatu kwenye msimamo msimu wa 2024/25 baada ya kucheza mechi 9 Novemba 6 2024 inatarajiwa kucheza mchezo wa ushindani dhidi ya KMC, Uwanja wa KMC, Mwenge.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata TUNAOMBA ODA 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.