TAMKO LA SIMBA BAADA YA KUPOTEZA KARIAKOO DABI

AHMED Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa kupoteza mchezo wao wa Kariakoo Dabi ni maumivu kwao ila wanajipongeza kwa kutengeneza timu mpya ambayo inawapa matokeo mazuri.

Ikumbukwe kwamba Oktoba 19 2024 ilikuwa Simba 0-1 Yanga bao likipachikwa dakika ya 86 na mtupiaji ni Maxi Nzengeli hivyo Simba ilipoteza pointi tatu ikiwa nyumbani.

Kupitia ukurasa wa Instagram Ahmed Ally ameandika namna hii: “Tunaumia kwa kupoteza mchezo wa derby lakini tunajipongeza kwa kuwa mradi wetu wa kutengeneza timu umeanza kutoa matunda tena kwa haraka sana.

“Wote ni mashahidi misimu kadhaa nyuma tulifungwa derby na kuzidiwa kwa dakika zote 90. Tumeona tofauti kubwa, tumefungwa lakini tumeutawala mchezo kwa asilimia kubwa na kama kila kitu kingekua sawa basi tungeshinda mchezo ule.

“Muhimu kwetu wana Simba kwanza tukubali tumepoteza na wala hakuna haja ya kuanza kuhesabu tumepoteza mara ngapi, mpira ni maisha ya duara muda wetu utafika na sisi tutatawala derby kwani tumewahi kufanya hivyo.

“Muhimu kwa sasa ni kusahau yaliyotokea na kujipanga upya kwa vita iliyo mbele yetu. Tumebakiwa na michezo 24 nguvu kubwa iwe kushinda michezo hiyo, tumepoteza derby sio ubingwa. Na pia tuwekeze nguvu kwenye mchezo wetu Jumanne dhidi ya Tanzania Prisons.”

Ubaya Ubwela unaendelea..

USIKOSE kitabu kipya kilichoandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, kinaitwa kitabu cha Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kukipata 0756 028 371. Ni simulizi inayozungumzia maisha ya Kiafrika, usaliti, visa, furaha. Wakazi wa Njombe kitabu kinapatikana Mtaa wa Mpechi kwa Chris Jabari, Kigamboni kwa Tupokigwe, Posta karibu na Mnara wa Askari ukiwa unaelekea chuo cha IFM.