UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa umefurahia ushindi wao katika mchezo wa Mzizima Dabi uliochezwa Uwanja wa New Amaan Complex kwa kukomba pointi tatu muhimu kwenye mchezo huo.
Ni Septemba 26 2024 mchezo huo ulichezwa baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa New Amaan Complex ulisoma Azam FC 0-2 Simba mabao yakifungwa na Leonel Ateba dakika ya 14 na Fabrince Ngoma dakika ya 47.
Kila kipindi Simba ilifunga bao mojamoja ambapo umakini kwenye safu ya ushambuliaji kipindi cha kwanza ulikuwa mdogo kwa Simba kutokana na nafasi ambazo walizipata huku Azam FC ikionekana kwamba walitumia mbinu kubwa ya kujilinda kwenye mchezo huo na kushambulia kwa kushtukiza.
Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amebainisha kuwa walikuwa wanahitaji kupata pointi tatu muhimu na ilikuwa hivyo kutokana na mpango kazi ambao ulipangwa na mwisho wameibuka na ushindi jambo ambalo ni furaha kwao.
“Tumefurahi kupata ushindi kwenye mchezo wetu muhimu na ilikuwa hivyo kikubwa ni kwamba kila mchezaji alikuwa anatambua kwamba tunahitaji pointi tatu na walicheza kwa kujituma mwanzo mwisho kwa ajili ya kupata matokeo mazuri uwanjani wanastahili pongezi wachezaji wetu.
“Kazi bado inaendelea kwa kuwa tuna mchezo mwingine dhidi ya Dodoma Jiji hivyo wachezaji wakirudi Tanzania watakuwa na kazi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu ujao hivyo bado kazi kubwa tutaifanya ili kupata matokeo mazuri.”
Mechi tatu ambazo ni dakika 270 Simba imekomba pointi tisa safu ya ushambuliaji imefunga mabao 9 ikiwa na wastani wa kufunga mabao matatu kila baada ya dakika 90.
Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi kitabu cha Ganzi ya Maumivu,kukipata 0756 028 371