KIUNGO wa Azam FC inayotumia Uwanja wa Azam Complex kwenye mechi za nyumbani anafanya kile apendacho uwanjani kwa vittendo kutokana na kazi yake kuonekana ndani ya dakika 90 kwenye mechi ambazo anacheza.
Ndani ya Azam FC, Feisal Salum ni namba moja kwa watengeneza pasi za mwisho akiwa ametengeneza jumla ya pasi tatu za mabao kati ya matano yaliyofungwa na timu hiyo kwenye mechi tano za ligi ambazo ni dakika 450 ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 90.
Kiungo huyo alitoa pasi mbili mchezo dhidi ya KMC uliochezwa Septemba 19 2024 mwisho ubao ukasoma KMC 0-4 Azam FC. Ikumbukwe kwamba huu ulikuwa ni mchezo wa kwanza kwa Azam FC kupata ushindi ndani ya ligi msimu wa 2024/25 baada ya kucheza mechi mbili ambazo ni dakika 180 bila kupata ushindi.
Alimpa pasi mfungaji wa kwanza ndani ya Azam FC Nado ambaye alifunga bao hilo akiwa ndani ya 18 akitumia mguu wa kulia na pasi ya pili alimpa Lusajo Mwaikenda dakika ya 54 aliyefunga bao hilo akiwa ndani ya 18.
Pasi ya tatu alimpa mfungaji wa mabao magumu Azam FC, Saadun Nassoro dhidi ya Coastal Union dakika ya 9. Bao hili linaingia kwenye orodha ya mabao ya mapema kabisa kwa Azam FC kwenye ligi.
Kiugo huyo alipoulizwa hivi karibuni kipi anapenda kufanya akiwa uwanjani kati ya kufunga ama kutoa pasi Fei alisema: “Kwangu mimi napenda zaidi kutoa pasi za mabao.”