SIMBA: AZAM FC HAWAWEZI KUTUTISHA, TUNAOGOPESHA AFRIKA

UONGOZI wa Simba umebainisha kuwa wapinzani wao Azam FC ndani ya Ligi Kuu Bara hawawezi kuwatisha kwa kuwa wao wenyewe wanaogopesha Afrika.

Ipo wazi kwamba Simba ndani ya ligi ni mechi mbili imecheza ikishinda mechi zote ndani ya dakika 180 msimu wa 2024/25 ikiwa imekusanya jumla ya pointi sita kibindoni.

Azam FC ni mechi nne imecheza ushindi kwenye mechi mbili na sare kwenye mechi mbili ndani ya dakika 360.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amebainisha kwamba wanatambua umuhimu wa mchezo wa leo dhidi ya Azam FC lakini hawana hofu kuwakabili wapinzani wao ndani ya uwanja.

“Tunawaheshimu wapinzani wetu lakini hawatutishi kwani sisi tunaogopesha Afrika, tulicheza nao Uwanja wa Mkapa tukawafunga mabao matatu na hata tulipocheza visiwani tuliwafunga sasa waache waende popote sisi tunawafuata na tunakwenda kutafuta ushindi dhidi yao.”

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa New Amaan Complex ukiwa ni mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Bara kuchezwa hapo kwa wababe hawa wawili msimu wa 2024/25.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Mtunzi wa Ganzi ya Maumivu Kwenye Upendo, kuipata 0756 028 371.