AZAM FC MOTO HAUZIMI, MCHEZAJI BORA KATUPIA BAO LA KALI

MATAJIRI wa Dar, Azam FC moto hauzimi baada ya kupata ushindi kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya KMC Uwanja wa KMC Mwenge kasi yao imeendelea kwa mara nyingine mbele ya Coastal Union ya Tanga.

Azam FC ilicheza mechi mbili mfululizo bila kupata ushindi ilikuwa JKT Tanzania 0-0 Azam FC, Azam FC 0-0 Pamba Jiji na ushindi wa kwanza ilikuwa KMC 0-4 Azam FC na mchezo wa nne ilikuwa Azam FC 1-0 Coastal Union.

Huu ni mchezo wa kwanza kwa Azam FC kushinda ikiwa nyumbani ndani ya dakika 90 kwa msimu wa 2024/25 bao likifungwa na Nassor Saadun dakika ya 9 likiwa ni bao la mapema zaidi kufungwa na Azam FC msimu huu mpya.

Nyota huyo alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo na alitupia bao kali kwenye mchezo huo ambalo lilidumu mpaka mwisho wa mchezo wakikomba pointi tatu mazima.

Saadun amesema: “Namshukuru Mungu kwa ushindi na ninafurahi sana kuchukua tuzo hii ya mchezaji bora wa mchezo tunawashukuru mashabiki wa Azam FC kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo wetu.”

Saadun kwenye mchezo huo alikomba dakika 90 aligusa mpira mara 29 na mashuti mawili alipiga kuelekea langoni na moja lilikuwa bao la ushindi kwa mujibu wa rekodi za Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azam FC inafikisha pointi 8 nafasi ya tatu kwenye msimamo baada ya kucheza mechi nne vinara ni Singida Black Stars wenye pointi 12 hawa wameshinda mechi zote mfululizo.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Dizo Click