SIMBA: HATUTAKI KUISHIA HAPA, MALENGO NI MAKUNDI KIMATAIFA

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa kwenye anga la kimataifa katika Kombe la Shirikisho Afrika hawataki kuishia hatua ya pili bali malengo ni kuona kwamba wanatinga hatua ya makundi.

Kazi pekee inayohitajika kwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids ni kupata ushindi kwenye mchezo ujao dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Septemba 22 baada ya mchezo wa awali kusoma 0-0.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa mpango mkubwa uliopo kwa timu hiyo ni kusaka ushindi kwenye mchezo wao ujao na wanatambua inawezekana hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi.

“Wote mliona vijana wetu waliocheza kwa nidhamu pale Libya licha ya vurugu zote. Sasa ngoma inahamia nyumbani twendeni tukawape nguvu vijana wetu wakatupeleke hatua ya makundi. Jambo la kushinda ni la kila Mwanasimba. Mechi yetu ndio yenye mvuto zaidi Afrika wikiendi hii. Na sisi kama Mnyama hatutaki kuishia hatua hii kwa mapenzi yake Mwenyezi Mungu. Tunayo timu nzuri sana, tuna kikosi kizuri sana lakini pia viongozi wenu tumejipanga kuhakikisha Simba yetu inafuzu makundi.

“Lakini hatuwezi kufuzu bila ninyi mashabiki wa Simba kuungana kwa pamoja na kuujaza uwanja wa Mkapa basi Al Ahli Tripoli hana sehemu ya kutokea. Mechi ya kwanza pale Libya waliwafanyia sana vurugu wachezaji wetu lakini mimi hawakunigusa, waliniogopa, ukiniangalia natisha. Tuliona vitendo vingi vya ovyo ambavyo walifanya lakini sisi inabidi tuwe kinyume chao sababu sisi ni timu kubwa Afrika lakini pia sisi tumeshapewa Tuzo ya Mashabiki Bora Afrika. Kama unaweza kumuua adui yako kwa asali ya nini kutumia sumu?