AZAM FC YAIPIGIA HESABU KMC

UONGOZI wa Azam FC umebainisha kuwa upo tayari kwa mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC kutokana na maandalizi waliyofanya na wanahitaji pointi tatu muhimu.

Ikumbukwe kwamba kwenye mechi mbili za Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 Azam FC haijafungwa wala kufungwa ndani ya dakika 180 walizocheza mechi za ushindani uwanjani.

Hasheem Ibwe, U 17 ameweka wazi kuwa hakuna kinachowaumiza kama safu ya ushambuliaji kutofunga lakini suala la kutofungwa hilo ni habari njema kwao.

“Unaona tumecheza mechi mbili za ligi hatujafungwa wala hatujafunga, kwenye kutofungwa tunasema linapaswa kuendelea ila kwenye kufunga hapa ndipo tunataka kufanya kweli kwa kuwa ili kupata ushindi ni lazima ufunge.

“Mchezo wetu dhidi ya KMC ni muhimu na tunatambua kwamba watakuwa wanafikiria hatuhitaji ushindi hilo wasahau, tunawaheshimu na tunawafuata tukiwa na hesabu za kupata pointi tatu muhimu, mashabiki wajitokeze kwa wingi tupo tayari.”

Mechi mbili za Azam FC ilikuwa JKT Tanzania 0-0 Azam FC, Azam FC 0-0 Pamba Jiji. Mchezo dhidi ya KMC unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa KMC, Mwenge.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Dizo Click.