BENCHI la ufundi la Simba limebainisha kwamba limeshangazwa na vitendo vilivyofanyika na mashabiki wa Al Ahli Tripoli kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika huku wakipanga kulipa kisasi kwa mtindo wa kipekee ndani ya uwanja.
Ikumbukwe kwamba timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids, Septemba 15 ilikuwa na kazi kusaka ushindi ugenini baada ya dakika 90 ubao ulisoma Al Ahli Tripoli 0-0 Simba na mchezo wa marudio unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Septemba 22.
Fadlu amesema kuwa walishangazwa na vitendo vya mashabiki kwa kuwa havikuwa vya kimpira kabisa kwa kuwapa presha kubwa wakiwa uwanjani na muda wakutoka jambo ambalo sio sawa.
“Ulikuwa ni mchezo uliokuwa na mambo mengi unaona kwamba mashabiki wao walijitokeza wengi lakini walikuwa na vitendo ambavyo havikuwa vya kimpira hatujafurahishwa na hili ila tunaamini kwamba nasi tunakwenda kucheza nao Uwanja wa Mkapa ni muda wa mashabiki kujitokeza kwa wingi.
“Mchezo wetu utakuwa na ushindani mkubwa hilo lipo wazi lakini mashabiki wakijitokeza kwa wingi itaongeza nguvu kwenye kutafuta ushindi hilo linawezekana na tupo tayari kwa mchezo wetu ujao.”
Kwenye mchezo uliopita kiungo mkabaji Mzamiru Yassin, Ladack Chasambi hawa hawakuwa kwenye kikosi kilichokuwa Libya huku kiungo Yusuph Kagoma alipata nafasi ya kuanza kikosi cha kwanza.