VINARA WA LIGI KUU BARA WAIWAHI PAMBA JIJI MWANZA

VINARA wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 Singida Black Stars mapema wamewawahi wapinzani wao Pamba Jiji kwa lengo la kuzoea mazingira na kuanza mazoezi kuelekea mchezo wao wao ujao ambao utakuwa ni wannne.

Ipo wazi kuwa timu hiyo inayonolewa na Kocha Mkuu, Patrick Aussems baada ya kucheza mechi tatu ambazo ni dakika 270 ilishinda zote na kukomba pointi tatu mazima ikifikisha jumla ya pointi tisa ikiwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo.

Mchezo ujao ni dhidi ya Pamba Jiji unatarajiwa kuchezwa Septemba 17, Mwanza tayari kikosi cha Singida Black Stars chenye wachezaji 27 kimewasili Mwanza kamili kuwasubiri wenyeji wao ambao watakuwa na mchezo wa ligi dhidi ya Azam FC, Septemba 14, Dar.

Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussen Masanza amesema kuwa wamewahi mapema jiji la miamba kuanza maandalizi ya mchezo wao muhimu dhidi ya Pamba wakiwa kamili gado.

“Tayari vinara wa ligi tupo ndani ya jiji la miamba Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wetu dhidi ya Pamba Jiji na tunafahamu kwamba watakuwa na kazi nje ya Dar hilo tunalitambua tunataka wakija watukute tunawasubiri tayari kuelekea mchezo wetu ambao utachezwa Septemba 17.

“Wachezaji ambao walikuwa kwenye timu za taifa tayari wamesharejea kwenye kikosi ikiwa ni Marouf Tchakei, Mohamed Kamara, Victorien Adebayo, Tchakei na Kamara wameungana na timu Mwanza kwa ajili ya maandalizi ya mchezo ujao lakini Adebayo amebaki Singida kwa ajili ya program maalumu,”.

Mchezo uliopita ilikuwa ni Septemba 12 ubao wa Uwanja wa Liti baada ya dakika 90 ulisoma Singida Black Stars 2-1 KMC mabao ya Singida Fountain Gate yalifungwa na Bada Arthur
na Elvis Rupia huku kwa KMC mtupiaji akiwa ni Redemtus aliyeanzia benchi katika mchezo huo.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Dizo Click.