YANGA KAZINI KIMATAIFA LIGI YA MABINGWA AFRIKA

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye anga la kimataifa Yanga kesho Septemba 14 2024 wanakibarua cha kusaka ushindi kwenye mchezo dhidi ya CBE SA ya Ethiopia.

Septemba 12 2024 msafara wa Yanga uliwasili salama nchini Ethiopia kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo huo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kwa timu zote mbili.

Miguel Gamondi, Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo hivyo hesabu kubwa ni kupata matokeo mazuri katika mchezo wao wa kimataifa ambao ni muhimu.

“Tunatambua umuhimu wa mchezo wetu dhidi kwenye hatua hii ambayo tupo kikubwa ni kuona kwamba tunapata matokeo mazuri. Wachezaji wapo tayari na tutaingia uwanjani tukiwa na shauku ya kupata ushindi ndani ya uwanja tunaamini itakuwa hivyo kutokana na utayari ambao upo.

“Kwenye kila hatua kuna ushindani mkubwa hii hatua ambayo tupo ni tofauti na ile iliyopita tunalitambua hivyo na muda uliopo ni kupata matokeo mazuri.”

Yanga imetinga hatua ya pili kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa jumla ya mabao 10-0 dhidi ya Vital’O kwa ushindi wa nje ndani.

Miongoni mwa wachezaji waliopo Ethiopia ni Aziz Ki, Clement Mzize, Clatous Chama, Djigui Diarra.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka, Dizo Click.