UONGOZI wa Fountain Gate umeweka wazi kuwa mpango mkubwa ni kupata pointi tatu kwenye mechi zao zote ambazo watacheza kutokana na kuwa na kikosi bora.
Mechi mbili mfululizo Fountain Gate imekomba pointi tatu ilikuwa kwenye mchezo dhidi ya Namungo ugenini na mchezo dhidi ya Ken Gold wakiwa nyumbani.
Katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Majaliwa ilikuwa Namungo 0-2 Fountain Gate na mchezo wa pili kushinda ilikuwa Fountain Gate 2-1 Ken Gold ulichezwa Uwanja wa Tanzanite, Kwaraa.
Ofisa Habari wa Fountain Gate, Issa Liponda maarufu kama Mbuzi ameweka wazi kuwa kikosi kipo imara na mpango wao ni kupata pointi tatu kwenye mechi ambazo watacheza uwanjani.
“Tuna kikosi imara na chenye wachezaji wenye ari ya kupambana kikubwa ambacho tunakifanya ni kuwa bora kila tunapomaliza mchezo ili kupata pointi tatu muhimu kwenye mechi ambazo tunacheza hilo linawezekana na tunafanya hivyo kuwa bora kila wakati. Mashabiki wanapaswa kuelewa kwamba tupo kwa ajili ya kuwapa burudani.”
Mchezo wa kwanza kwa Fountain Gate iliyokusanya pointi sita kibindoni ndani ya dakika 270 ilikuwa dhidi ya Simba uliochezwa Uwanja wa KMC ilishuhudia ubao ukisoma Simba 4-0 Fountain Gate.