>

WACHEZAJI STARS WAPEWA PONGEZI USHINDI AFCON

BENCHI la ufundi la timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars limeweka wazi kuwa pongezi kubwa kwa ushindi wa mchezo wa kuwania kufuzu AFCON 2025 mbele ya Guinea wanastahili wachezaji kwa kuwa walicheza kwa kujituma na kufuata malekezo.

Ni Septemba 10 2024 Stars ikiwa ugenini ilikomba pointi tatu mazima mbele ya Guinea wakipindua meza kibabe baada ya kuanza kufungwa kwenye mchezo huo kipindi cha pili ambapo Ally Salim aliyeanza langoni alitunguliwa bao moja.

Juma Mgunda, kocha msaidizi wa Taifa Stars amesema kuwa ulikuwa ni mchezo wenye ushindani mkubwa kwa kuwa wapinzani wao Guinea ni bora uwanjani na walionyesha ushindani wa kweli mwisho ushindi ulikuwa upande wao.

“Ulikuwa ni mchezo mgumu na wenye ushindani mwisho ushindi umekuwa upande wa Tanzania, pongezi kubwa kwa wachezaji kwani wamepambana kufuata maelekezo na kupata matokeo mazuri ambayo yanatupa nguvu kuelekea mchezo ujao baada ya mapumziko ambayo tutakuwa nayo.

“Ipo wazi kwamba tuna mechi nyingine mbili dhidi ya DR Congo, makosa tutafanyia kazi tutakwenda uwanja wa mazoezi kufanyia maboresho yale ambayo tulishindwa kwenda nayo sawa lakini kila mmoja ameona.” amesema Mgunda.

Ni Mohamed Bayo alianza kupachika bao dakika ya 57, usawa uliwekwa na Feisal Salum dakika ya 61 na bao ka ushindi likifungwa na Mudathir Yahya dakika ya 88.

Imeandikwa na Lunyamadzo Mlyuka