MWAMBA AHOUA AMELETA BALAA FOUNTAIN GATE

KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Jean Ahoua ameushtua uongozi wa Fountain Gate baada ya bao lake la kwanza ndani ya Ligi Kuu Bara kutajwa kuwa ni miongoni mwa bao bora katika mchezo huo.

Ukiweka mbali uongozi wa Fountain Gate kupitia kwa Ofisa Habari, Issa Liponda kutaja kuwa hilo ni bao pekee ambalo lilikuwa katika mipango makini asilimia kubwa ya mashabiki waliojitokeza Uwanja wa KMC, Mwenge Agosti 25 2024 walilitaja bao hilo kuwa bora.

Ikumbukwe kwamba baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa KMC, Mwenge ulisoma Simba 4-0 Fountain Gate, mabao yakifungwa na Edwin Balua dakika ya 13, Steven Mukwala dakika ya 44, Ahou dakika ya 58 na Valentino Mashaka dakika ya 81.

Liponda amesema:” Ulikuwa ni mchezo mzuri na bahati mbaya tumepoteza ila tungekuwa na wachezaji wetu wote kikosini tusingetoka kinyonge. Bao pekee ambalo nimeliona angalau likanishtua ni la Ahoua hayo mengine hata sijui nani amefunga.

“Tuna timu imara ambayo inajengwa na inawapongeza wachezaji wetu kwa namna ambavyo wanapambana kwenye kutimiza majukumu, bado tupo imara na sasa tunakwenda kufanyia kazi makosa ambayo yametokea kwenye mchezo wetu kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Namungo ambao utachezwa Uwanja wa Majaliwa.”

Katika mchezo huo uliochezwa Agosti 25 2024 wakati Simba ikikomba pointi tatu mazima, Ahoa alichaguliwa kuwa mchezaji bora akitoa pasi mbili za mabao na kufunga bao moja kwenye mchezo huo. Pasi ya kwanza alimpa Balua aliyefunga bao la ufunguzi kwa pigo la kichwa akiwa ndani ya 18.