>

AZAM WAMSAJILI ‘MBAPPE’ KUTOKA REAL BAMAKO

KLABU ya Azam FC imethibitisha kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji wa Kimataifa wa Mali, Cheickna Diakite, waliyemnunua kutoka miamba ya huko kwao, Real Bamako kwa mkataba wa miaka mitatu.

Azam FC inakwenda kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2024/25 ambapo itaanzia hatua ya awali baada ya kugotea nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi 2023/24.

Chini ya Kocha Mkuu, Yusuph Dabo imeweka kambi Morocco ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

“Nyota huyo chipukizi, 19, aliyepachikwa jina la staa wa Real Madrid, Mbappe kutokana na kasi na uwezo wake wa kuipenya safu ya ulinzi ya timu pinzani, amesaini mkataba wa miaka mitatu utakaomfanya kudumu ndani viunga vya Azam Complex hadi mwaka 2027.” imeeleza taarifa ya Wanalambalamba hao.