MATAJIRI WA DAR WAENDELEZA KAZI ZANZIBAR

MATAJIRI wa Dar, Azam FC wameweka kambi Zanzibar ikiwa ni mwendelezo wa maandalizi ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2024/25 pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.

Azam FC chini ya Kocha Mkuu Yusuph Dabo ina kibarua cha kupeperusha bendera kwenye anga la kimataifa jambo ambalo linafanyiwa kazi kwa umakini ili kupata matokeo mazuri kitaifa na kimataifa.

Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC amebainisha kuwa wanatambua umuhimu wa kufanya vizuri kwenye mashindano ambayo wanashiriki jambo ambalo linawafanya waendelee na maandalizi kwa ajili ya msimu wa 2024/25.

Tayari Azam FC wamewasili kambini Zanzibar na walianza mazoezi mara baada ya kuwasili Kisiwanj Unguja, Zanzibar, usiku wa Julai 9 waliendelea na programu ya mazoezi.

Ibwe amesema: “Mwendelezo wa maandalizi kwa ajili ya msimu mpya, tumewasili salama Zanzibar tukiwa na benchi la ufundi pamoja na wachezaji wetu wote kuelekea msimu mpya. Tupo tayari na tunaamini kwamba tutakuwa na muda mzuri wa maandalizi.”

Azam FC walianza maandalizi kwa kutumia Uwanja wa Azam Complex, Dar na sasa wapo Zanzibar wanatarajia pia kukwea pipa kwenda nje ya Tanzania ikiwa ni mwendelezo wa maandalizi.

Miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Azam FC ni Yanick Bangala, Feisal Salum maarufu kama Fei Toto.