AZAM FC YAMALIZANA NA MTAMBO WA MABAO

WAWAKILISHI wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, Azam FC inayonolewa na Kocha Mkuu, Yusuph Dabo wamemalizana na mtambo wa mabao kutoka Mashujaa kwa ajili ya changamoto mpya ndani ya timu hiyo.

Ikumbukwe kwamba msimu wa 2023/24 Azam FC ilimaliza ligi ikiwa nafasi ya pili na pointi 69 baada ya kucheza mechi 30 itapeperusha bendera ya Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pamoja na mabingwa Yanga.

Ni Adam Adam ambaye alikuwa mshambuliaji chaguo la kwanza ndani ya Mashujaa ametambulishwa Azam FC kwa dili la mwaka mmoja kuwa kwenye viunga vya matajiri hao wa Dar.

Taarifa kutoka  Azam FC zimeeleza namna hii: “Baada ya kucheza miaka 10 nje ya viunga vya Azam Complex, hatimaye tumemrejesha kijana wetu Adam Adam.

“Tunathibitisha kuwa tumeingia naye mkataba wa mwaka mmoja, tayari kabisa kuitumikia Azam FC msimu ujao 2023/24.

“Adam msimu uliopita alifanikiwa kufunga jumla ya mabao saba kwenye ligi, alipokuwa na kikosi cha Mashujaa.

“Mshambuliaji huyo ni moja ya zao la Akademi ya Azam FC, aliyojiunga nayo mwaka 2011-2014, ikiwa chini ya kocha, Vivek Nagul na kubeba baadhi ya mataji kama vile U-20 Uhai Cup na Rollingstone.”