MWAMBA HUYU HAPA KABEBA TUZO MEI

KATIKA mechi 7 ambazo ni dakika 630 Koch Mkuu wa Simba Juma Mgunda alikomba jumla ya pointi 19 ndani ya uwanja.

Ni ushindi katika mechi sita na aliambulia sare moja ugenini ilikuwa Uwanja wa Kaitaba alipokomba pointi moja.

Mechi zake ilikuwa ni Simba 2-0 Mtibwa Sugar, Simba 2-0 Tabora United, Azam FC 0-3 Simba, Simba 4-1 Geita Gold, Simba 1-0 KMC, Simba 2-0 JKT Tanzania na sare ilikuwa Kagera Sugar 1-1 Simba.

Mgunda amechaguliwa kuwa kocha bora ndani ya Mei akiwashinda Miguel Gamondi wa Yanga na Bruno Ferry wa Azam FC alioingia nao fainali kwa mujibu wa taarifa kutoka Kamati ya Tuzo ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF).

Upande wa mchezaji bora ni Reliants Lusajo mshambuliaji wa Mashujaa ya Kigoma ambapo aliwashinda Feisal Salum wa Azam FC na Aziz Ki wa Yanga.

Ndani ya Mei Lusajo alitimiza majukumu yake vema katika mechi nne akiwa chachu ya ushindi kati ya mechi sita ambazo Mashujaa ilishuka uwanjani.

Mashujaa ilikomba pointi 12 na ilipanda katika msimamo wa ligi ikimaliza nafasi ya 8 msimu wa 2023/24.

Mwamba huyo rekodi zinaonyesha kuwa alikomba dakika 432 katika mechi 6 alifunga mabao matano na pasi mbili za mabao akihusika kwenye mabao 7.