SIMBA YATAJA SABABU YA HUZUNI KUTAWALA

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa ni huzuni kubwa imetawala kwa wakati huu kutokana na kushindwa kufikia malengo yao kwa asilimia kubwa msimu wa 2023/24.

Ipo wazi kuwa ni namba tatu imegotea kwenye ligi ikiwa na pointi 69 tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga dhidi ya Azam FC iliyomaliza ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo. CRDB Federation Cup imepishana nalo kama ilivyokuwa kwenye taji la ligi.

Ukuta ule wa Simba wenye Che Malone baada ya mechi 30 ambazo ni dakika 2,700 uliruhusu mabao 25 na safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 59.

Wakati Simba ikishuhudia taji la ligi likiwa mikononi mwa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika iligotea hatua ya robo fainali ikikwama kutwaa taji hilo kubwa Afrika na iliposhiriki African Football Cup iligotea hatua ya robo fainali.

Simba ni mashuhuda wa bingwa mpya wa CRDB Federation Cup kuwa ni Yanga iliyoshinda kwa penalti 6-5 dhidi ya Azam FC kwenye fainali iliyochezwa Juni 2 2024, Uwanja wa New Amaan Complex..

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa ulikuwa ni msimu wenye ushindani mkubwa na matarajio yao yote hayajatimia jambo linalowapa masikitiko.

“Tuna majonzi makubwa kwa wakati huu ninatambua kwamba Wanasimba hawajafurahi namna ambavyo tumamaliza, haya ni masikitiko kwetu hatujafikia malengo yetu kwa asilimia kubwa hilo lipo wazi. Nyakati zinabadilika hivyo tunaamini kwamba tutarejea tukiwa imara.

“Bado tuna muda wakufanyia kazi makosa ambayo yalipita kwa ajili ya kuwa imara wakati ujao, mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi mambo mazuri yanakuja na tutafanya vizuri katika wakati ujao.”