MCHEZAJI BORA FAINALI CRDB FEDERATION CUP AKIRI HAIKUWA RAHISI

KITASA wa kazi ndani ya Yanga ambaye ni beki chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Miguel Gamondi amebainisha kuwa haikuwa rahisi kwenye mchezo wa fainali ya CRDB Federation Cup.

Ni Ibrahim Abdullah ‘Bacca’ ambaye baada ya mchezo kukamilika alichaguliwa kuwa Mchezaji Bora mechi ya fainali hiyo iliyochezwa Uwanja wa New Amaan Complex.

Kazi kubwa aliyofanya kwenye mchezo huo akishirikiana na wachezaji wengine wa Yanga ilikuwa kuzuia hatari za wachezaji wa Azam FC wakiongozwa na Feisal Salum kumtungua Djigui Diarra ambaye alikuwa salama kwa muda mrefu ndani ya dakika 120.

Yanga ilitwaa taji hilo kwa ushindi wa penalti 6-5 baada ya dakika 120 ngoma kuwa nzito kwa pande zote kukwama kupata nafasi ya kufunga ndani ya uwanja kwenye muda wa kawaida.

Beki huyo amekomba milioni moja kutoka kwa wadhamini CRDB  ambayo inakuwa ni mali yake akibainisha kuwa ni zawadi kwa familia yake iliyoshuhudia yote yakitokea

“Ilikuwa ni kazi kubwa kwani nina amini hata nyinyi ni mashuhuda wa mchezo huo ikiwa hivyo kwa kuwa fainali ilikuwa ngumu mpaka mshindi kupatikana kwa penalti.

“Kuwa mchezaji bora wa mechi ni furaha kwangu na zawadi hii inakuwa kwa familia yangu kwa kuwa wamekuja kushuhudia namna kazi ilivyokuwam nawashukuru mashabiki kwa namna ambavyo wamejitokeza.”