YANGA WANA JAMBO LAO NA AZAM FC

MABINGWA watetezi wa CRDB Federation Cup, Yanga chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi wana jambo lao na Azam FC kwenye mchezo wa fainali.

Ngoma inatarajiwa kuchezwa leo ndani ya dakika 90 katika msako wa mshindi mpya ikiwa ni mchezo wa funga msimu wa 2023/24.

Ipo wazi kwamba Yanga wana taji la Ligi Kuu Bara walitwaa wakiwa na mechi tatu mkononi kwa kuwa walipopata ushindi mchezo wa 27 dhidi ya Mtibwa Sugar walifikisha pointi 71 ambazo hazijafikiwa na timu yoyote Bongo.

Kikosi hicho kipo tayari kwa mchezo wa leo dhidi ya Azam FC na miongoni mwa wachezaji ambao wapo  tayari ni kiungo mshambuliaji wa Yanga Aziz KI ambaye ni mkali kwenye kucheka na nyavu.

Ikumbukwe kwamba kwenye ligi msimu wa 2023/24 kwenye mzunguko wa kwanza Ki aliwafunga hat trick Azam FC akiwa ni namba moja kwa utupiaji baada ya kufunga mabao 21.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema: “Wachezaji wote wapo tayari kwa fainali ikiwa ni pamoja na masta KI, Maxi Nzengeli, Bakari Mwamnyeto, tunatambua ni mchezo mgumu lakini tutafanya kazi kubwa kupata matokeo.”