SIMBA WATOA YA MOYONI, KUREJEA KWENYE UBORA

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa utafanyia kazi makosa ambayo yamepita ili kurejea kwenye ubora wao kwa kuwa nyakati ambazo wamepita zimewaumiza.

Ipo wazi kuwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Juma Mgunda imegotea nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 69.

Imepishana na taji la ligi pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika na inakwenda kushuhudia bingwa mpya wa CRDB Federation Cup akipatikana leo kati ya Azam FC na Yanga, fainali inayotarajiwa kuchezwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba ameweka wazi kuwa nyakati ambazo wamepitia ni ngumu na hazijawafurahisha hivyo wanapambana kurejea kwenye ubora.

“Hatujapenda na tumekuwa na huzuni kwa kuwa tumepoteza kila kitu ambacho tulikuwa tunakipigania kwenye msimu ulioisha.

“Yote kwa yote yaliyopita tunayachukua na tunakwenda kuyafanyia kazi kwa ajili ya kuwa bora wakati ujao mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi.”

Ni Kombe la Shirikisho Simba itashiriki pamoja na Coastal Union huku Yanga na Azam FC zikiwa ndani ya Ligi ya Mabingwa Afrika.