MWAKINYO AFUNGUKIA ISHU YAKE NA AZAM

BONDIA Mtanzania, Hassan Mwakinyo amewaomba radhi mashabiki wake kwa sintofahamu iliyojitokeza usiku wa Ijumaa ya Mei 31, katika ukumbi wa Warehouse Masaki ambako alitarajiwa kupigana na Mghana, Patrick Allotey na jambo hilo kushindikana dakika za mwisho za usiku ule.

Kutokana na sintofahamu hiyo, Mwakinyo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii, amesema hakuna shida yoyote kati yake na Azam TV na kuongeza kuwa chombo hicho cha habari kilijitahidi sana kuhakikisha kile kilichotokea Ijumaa, kisitokee.

“NAOMBA NIANDIKE KWA HERUFI KUBWA YA KWAMBA AZAM TV HAWANA CHUKI WALA BIFU YOYOTE NA MIMI kama inavyo tafsiriwa na wengi, binafsi kilichotokea juzi wamejitahidi sana kupambana kisitokee nimeona jitihada zao kubwa sana zikifanyika kunusuru lile pambano kuanzia ngazi za juu mpaka chini ya uongozi.” ameandika Mwakinyo.

Pambano hilo lilifanyika tena jana na Mwakinyo kufanikiwa kuibuka mshindi kwa kumchapa Patrick Allotey kwa TKO, baada ya Mghana huyo kushindwa kuendelea na pambano akisema kuwa bega lilikuwa linamuuma punde baada ya kukamilika raundi ya pili.

Ushindi huo wa Mwakinyo umemwezesha mkali huyo wa masumbwi kuutetea Ubingwa wa Afrika Mkanda wa WBO.