MATAJIRI AZAM FC WATUMA UJUMBE HUU YANGA

MATAJIRI wa Dar, Azam FC wamebainisha kwamba wapo tayari kwa mchezo wa fainali dhidi ya Yanga inayonolewana Kocha Mkuu, Miguel Gamondi.

Azam FC inanolewa na Msenegal, Yusuph Dabo ambaye ameongoza kikosi hicho kumaliza kikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi.

Ni pointi 69 wamekomba Azam FC baada ya kucheza mechi 30 mchezo wao wa funga kazi ilikuwa Geita Gold 0-2 Azam FC ambapo moja ya bao lilifungwa na kiungo mshambuliaji Feisal Salum.

Feisal ambaye alifunga msimu akiwa na mabao 19 kwa 2023/24 ikiwa ni msimu wake wa kwanza kuwa ndani ya Azam FC akitokea Yanga kwenye mchezo wa ligi mzunguko wa pili aliwafunga mabosi wake hao wa zamani alipomtungua Djigui Diarra.

Leo wanatarajiwa kukutana kwenye fainali ya CRDB Federation Cup, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kwenye msako wa mshindi wa taji hilo ambalo lipo mikononi mwa Yanga.

Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC amesema kuwa kila kitu kipo sawa na wanatambua umuhimu wa mchezo huo hivyo watapambana kufanya vizuri.

“Tunatambua umuhimu wa mchezo wetu tutaingia kwa hesabu nzuri kusaka matokeo huku tukiwaheshimu wapinzani wetu kikubwa itakuwa ni fainali nzuri na mchezo utachezwa kwa umakini.”