MABINGWA YANGA WATEMBEZA MKWARA

MABINGWA wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2023/24 Yanga wametembeza mkwara mwingine kwa kubainisha kwamba hesabu kubwa ni kutwaa taji la CRDB Federation mbele ya Azam FC.

Ikumbukwe kwamba Yanga ni mabingwa watetezi wa taji hilo walitwaa mbele ya Azam FC kwenye fainali iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani kwa ushindi wa bao 1-0 huku mtupiaji akiwa ni Kennedy Musonda.

Juni 2 2024 fainali ya CRDB Federation inatarajiwa kuchezwa Uwanja wa New Amaan Complex huku timu zote zikiwa na uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika hesabu ni kutwaa taji hilo la kufungia msimu wa 2023/24.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa mipango ni endelevu kwenye kutwaa kila taji walilobeba msimu uliopita ikiwa ni pamoja na CRDB Federation.

“Tunakazi kubwa kuendelea kutimiza malengo yetu kama ambavyo tulibainisha mwanzo kwamba tunahitaji taji la ligi na sasa hesabu ni kuona kwamba tunatwaa CRDB Federation Cup.

“Kila mchezaji yupo tayari na benchi la ufundi linatambua umuhimu wa mchezo wetu, kikubwa ni kuwa pamoja kuelekea kwenye fainali yetu, mashabiki tuzidi kuwa pamoja kila kitu kinakwenda kuwa sawa.”