CHINI ya Kocha Mkuu, Yusuph Dabo kikosi cha Azam FC kinatarajiwa kushuka Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuwania tiketi ya kutinga hatua ya fainali dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Hesabu kubwa za Azam FC ni kupata ushindi kwenye mchezo huo ili kutwaa taji la CRDB Federation Cup ambalo lipo mikononi mwa Yanga.
Ikumbukwe kwamba Yanga ilishinda taji hilo kwa kuwatungua Azam FC bao moja kwenye mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Hasheem Ibwe, Ofisa Habari wa Azam FC ameweka wazi kwamba wanahitaji kufanya vizuri kwenye mechi zao zote kwa kuwa wapo tayari kupata matokeo.
“Tuna dhamira kubwa ya kupata matokeo kwenye mechi ambazo tunacheza hilo lipo wazi hivyo wapinzani wetu wawe tayari kwa ajili ya ushindani.”.
Azam FC ilianza kupata ushindi wa mabao 2-1 Alliance raundi ya pili, Azam FC 5-0 Green Warriors raundi ya tatu, Azam FC 3-0 Mtibwa Sugar raundi ya nne na katika robo fainali iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 Namungo.
Ni Mei 18 2024 mchezo huo unatarajiwa kwa wababe hao wawili kukutana uwanjani kusaka mshindi atakayetinga hatua ya fainali.
Kwa upande wa Coastal Union wao ilikuwa Coastal Union 2-0 Greenland, Coastal Union 1-0 Mbeya Kwanza, Coastal Union 0-0 JKT Tanzania ikashinda kwa penalti 5-4 katika raundi ya nne na robo fainali ilikuwa Coastal Union 1-0 Geita Gold.