IBRAHIM Bacca beki wa kazi ngumu ndani ya kikosi cha Yanga ameweka wazi kuwa benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi linafanya kazi kubwa kuwasoma wapinzani na kubadili mipango kwenye mchezo husika.
Ipo wazi kuwa kwenye mchezo wa mzunguko wa pili dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa Uwanja wa Azam Complex iliwabidi Yanga kusubiri mpaka dakika ya 83 kupata bao la ushindi.
Ilikuwa Mei 9 2024 ubao wa Uwanja wa Azam Complex ulisoma Yanga 1-0 Kagera Sugar bao la ushindi likifungwa na Mudathir Yahya.
Bacca amesema: “Tunamshukuru Mungu kwa kupata ushindi kwenye mechi zetu na kikubwa ni mbinu za benchi la ufundi namna ambavyo linafanya kazi kubwa.
“Kwenye mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar tulishindwa kutumia nafasi ambazo tulizipata mwanzo na mwishoni kabisa tukapata ushindi ilikuwa kazi kubwa kwetu na wachezaji tulipambana.
“Mwalimu alibadilisha mbinu kidogo kwenye mchezo wetu kisha nafasi ambayo tulipata tukaitumia na kupata ushindi kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar.”
Yanga ni namba moja kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 68 baada ya kucheza mechi 26 msimu wa 2023/24.