NAIBU Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Hamis Mwinjuma amewapa tano viongozi wa Yanga kwa kuandaa usafiri wa basi kwa ajili ya mashabiki kuelekea Afrika Kusini.
Yanga inatarajiwa kucheza mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns baada ya ule wa mkondo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa kutoshana nguvu bila kufungana.
Mwinjuma amesema: “Kwanza niwapongeze sana kwa uamuzi wa kusafiri kwa basi kwani mngeweza kusema mbaki nyumbani na kutazama mechi kwenye Tv, Hii inamaanisha nyinyi ni wafia Yanga, Hongereni sana.
“Uzuri kiwango cha timu yetu mmekiona na kinaridhisha, mpinzani tunayekwenda kucheza naye hana faida ya Mashabiki wengi hivyo naamini Nguvu ya kushangilia ambayo mnayo itakwenda kuleta tija kwenye mchezo wetu siku ya ijumaa.
“Nimekuja hapa kufikisha salamu za Serikali chini ya Daktari Samia Suluhu Hassan, kila kinachoendelea yeye anafuatilia kwa umakini na anawatakia kila la heri kwenye Safari hii na kwenye mchezo wetu siku ya ijumaa,”.