YANGA HAINA HOFU NA MAMELODI KWAO AMANI TU

UONGOZI wa Yanga umebainisha kwamba hauna tatizo na wapinzani wao kwenye anga la kimataifa Mamelodi Sundowns kwa kuwa vita yao ni ndani ya dakika 90 uwanjani.

Yanga wameweka wazi kuwakama kuna mashabiki wao ambao wapo Tanzania wajitokeze kwa wingi uwanjani kikubwa ni kuona wanapata burudani kwenye mchezo huo wa kimataifa unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Yanga inayonolewa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi ina kibarua cha kusaka ushindi ndani ya dakika 90 kwenye hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika ikisaka tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa maandalizi makubwa yanafanyika kwa timu hiyo kuelekea Machi 30 na malengo ni kupata matokeo chanya kuelekea mchezo huo ambao unasubiriwa kwa shauku kubwa.

“Sisi hatuna vita na Mamelodi, hatuwachukii, kama wapo wengi waje kwa wingi uwanjani. Young Africans SC lugha yetu ni amani, hatupigi wala kuzuia mtu kuja kwa Mkapa. Kama mnataka kwenda kuwapokea ndugu zenu nendeni wanafika Alhamisi. Ugomvi wetu na Mamelodi utakuwa kwenye Dakika 90 Uwanjani. Wote mnakaribishwa kwa Mkapa.

“Tunatambua ni mchezo mgumu na mashabiki wanatambua umuhimu wa kupata ushindi kwenye mchezo huo hivyo wajitokeze kwa wingi kushuhudia mchezo wetu ambao ni mkubwa,”.