WAKIWA kwenye maandalizi kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy, Simba imepeta mbele ya wakusanya mapato kutoka Kilimanjaro.
Kwenye mchezo wa raundi ya tatu iliambulia ushindi wa mabao 6-0 TRA Kilimanjaro katika mchezo wa Azam Sports Federation Cup.
Katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Azam Complex ni Ladack Chasambi alifungua kurasa za mabao katika mchezo huo.
Sadio Kanoute alifunga mabao matatu akisepa na mpira wake huku Pa Jobe na Fred Michael Kila mmoja alifunga bao mojamoja.
Chasambi alianza kufunga dakika ya 13, Kanoute bao la kwanza alifunga dakika ya 40, dakika ya 52 na dakika ya 54 alikamilisha hat trick yake ya kwanza akiwa na uzi wa Simba.
Fred alipachika bao dakika ya 51 na Jobe aliyeanzia benchi kwenye mchezo huo alifunga bao dakika ya 72 kwenye mchezo huo ambao wakusanya mapato walikusanywa jumlajumla na Simba.
Huu ni ushindi mkubwa kwa Simba ndani ya msimu wa 2023/24 kwenye mechi za ushindani.