NGOMA NZITO, POLISI TANZANIA YAWAPIGA MKWARA YANGA

MABINGWA watetezi wa Kombe la Azam Sports Federation Yanga leo wanakibarua cha kusaka ushindi kwenye mchezo wa raundi ya tatu.

Februari 19 kuna mechi ambazo zilichezwa katika raundi ya tatu na matokeo ilikuwa  Coastal Union 1-0 Mbeya Kwanza,  Singida FG 2-0 FGA Talents na Dodoma Jiji 2-1 Biashara United leo ni zamu ya Yanga.

Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga amesema kuwa wakati wanaendelea na kampeni kuelekea kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika wanatambua umuhimu wa mchezo wao dhidi ya Polisi Tanzania.

Polisi Tanzania wameweka tambo kupitia ukurasa wao wa Instagram, wakikitoa onyo kwa Yanga ya kwamba ni bora wangeomba mechi hiyo iahirishwe ili wajiandae na mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya CR Belouizdad inayotarajiwa kuchezwa Jumamosi.

“Bora wangedeka tu, lakini kwa vile wamekubali wenyewe hawataamini macho yao. Katika kipindi kama hiki tutawatupa rumande mpaka Jumamosi bila dhamana na hatuogopi kutupiwa yale mavitu yao,” ilieleza taarifa hiyo.

Yanga ilitwaa taji hilo kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC kwenye mchezo wa fainali uliochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.