TABORA UNITED YAINGIA CHIMBO KUIWINDA AZAM FC

WAKALI kutoka Tabora, kikosi cha  cha  Tabora United  kimeanza maandalizi kwa ajili ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya NBC Soka Tanzania Bara ambapo mchezo wao ujao itakuwa dhidi ya Azam FC.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Februali 19 2024 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Mjini Tabora.

Kikosi hicho cha nyuki wa Tabora kimeanza mazoezi ikiwa ni mara baada ya kutoka kumaliza mzunguko wa kwanza kwa mchezo dhidi ya Namungo na kutoka sare ya kufungana bao 1-1 moja huku lile la Tabora United likifungwa na Erick Okutu.

Tabora United chini ya kocha Mkuu ,Goran Copnovic inaendelea kujifua ili kujiweka vizuri kwenye michezo ya mzunguko huo wa pili wa Ligi kuu ya NBC Tanzania Bara pamoja na michuano ya Kombe la Azam Sport Federation ASFC.

Ofisa Habari wa Tabora United, Christina Mwagala amesema: “Tumemaliza mzunguko wa kwanza na Namungo na sasa tunajiandaa na mzunguko wa pili ambapo tutakutana na Azam FC Februali 19, na hali ya kikosi iko vizuri hivyo tunazidi kujipanga.

“Mzunguko wa kwanza umemalizika tukiwa na jumla ya alama 16, hatuko vizuri kimahesabu kulingana na malengo ambayo tulikuwa tumejiwekea kama Timu, lakini bado tuna nafasi ya kufanya vizuri kwenye michezo iliyopo mbele yetu.

“Aidha kwa upande wa Afya za wachezaji  kuna majeruhi wawili ambao ni Kevin Pemba Kingu na Erick Okutu mfungaji wa bao dhidi ya Namungo ambaye alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia huku kipa namba moja John Noble akisumbuliwa na Malaria,” amesema.