LEO ni leo kwa wakali kwenye mapigo ya penati kukutana kwenye mchezo wa hatua ya fainali ya Mapinduzi 2024 , Zanzibar.
Ipo wazi kwamba ni Mlandege ambao ni mabingwa watetezi dhidi ya Simba wenye shauku ya kutwaa taji hilo na rekodi zinaonyesha kwamba timu zote zilitinga hatua ya fainali kwa kushinda kwa penati katika hatua ya nusu fainali.
Hapa tunakuletea balaa lao lilivyokuwa namna hii:-
Mlandege mwendo wao
Desemba 30 2023, Mlandege 0-0 Azam FC, Desemba 30 2023, Mlandege 1-1 Vital’O bao la Mlandege lilifungwa na Optatus Lupekenya dakika ya 45 akiwa ndani ya 18 kwa mguu wa kushoto.
Mlandege 1-1 Chipukizi ilikuwa Januari Mosi 2024 na bao la Mlandege lilifungwa na Khori Bennet dakika ya 15 kwa mguu wa kulia akiwa ndani ya 18 dakika ya 15.
Hatua ya robo fainali Mlandege ilikuwa ni Januari 7 ubao ulisoma KVZ 0-0 Mlandege katika hatua ya mikwaju ya penalti ilikuwa ni KVZ 2-3 Mlandege.
Nusu fainali ya utata
Kwenye hatua ya nusu fainali ilizua utata kutokana na wapinzani wao APR FC kueleza kuwa wameonewa kwenye mchezo huo ilikuwa ni Januari 9. Katika dakika 90 ngoma ilikuwa Mlandege 0-0 APR FC. Mshindi alipatikana kwa penalti. Mlandege 4-2 APR FC.
Kadi nyekundu
Kadi nyekundu mbili zilitolewa kwenye mchezo huu ambapo ni Masoud Juma wa Mlandege na Nyigena Clement wa APR ilikuwa dakika ya 83 kwa kile ambacho mwamuzi alitafsri kuwa walikuwa wakileta fujo uwanjani kwa kutaka kupigana.
Januari Mosi JKU 1-3 Simba ni Moses Phiri dakika ya 8, Mohamed Hassan alijifunga dakika ya 64, Saleh Karabaka dakika ya 65 walifungwa bao la kwanza kwenye Mapinduzi 2024 na Neva Kaboma dakika ya 41.
Kwenye mchezo huu langoni alianza Ayoub Lakred ambaye alitunguliwa bao hilo katika hatua ya makundi.
Januari 3, 2024 Simba 2-0 Singida Fountain Gate, mabao yalifungwa na Willy Onana dakika ya 47 na Luis Miquissone dakika ya 59. Katika mchezo huu ni Ally Salim alianza kikosi cha kwanza na alikomba dakika 90 bila kuruhusu nyavu za Simba kutikiswa.
Januari 5 2024 Simba 0-0 APR wakati wakigawana pointi mojamoja ni Hussein Abel alianza langoni ambapo alikomba dakika 90 bila kutunguliwa akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mchezo.
Ilitinga hatua ya robo fainali na Januari 8 Simba 1-0 Jamhuri na bao lilifungwa na Jean Baleke dakika ya 45. Lakred alianza kikosi cha kwanza langoni.
Januari 10, hatua ya nusu fainali ilikuwa Singida Fountain Gate 1-1 Simba, Fabrince Ngoma alifunga bao kwa Simba dakika ya 90+8 lile la Singida Fountain Gate ni Elvis Rupia alifunga dakika ya 11.
Ushindi wa Simba ulipatikana kwa mikwaju ya penalti ilikuwa ni Singida Fountain Gate 2-3 Simba langoni ni Salim alianza.
Mabao
Safu ya ushambuliaji ya Simba ni mabao saba ilitupia kwenye mechi tano ambazo ni dakika 450 ikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila baada ya dakika 90. Ukuta uliokota mabao mawili.
Mlandege kwenye mechi tano ambazo walicheza jumla safu ya ushambuliaji ilitupia mabao mawili na ile ya ulinzi iliokota kibibindoni mabao mawili.