UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa bado upo imara kwa ajili ya mashindano mengine licha ya kufungashiwa virago kwenye Kombe la Mapinduzi 2024.
Ipo wazi kuwa Yanga iligotea hatua ya robo fainali baada ya kushuhudia ubao ukisoma Yanga 1-3 APR FC. Watakuwa mashuhuda wa fainali ya Mapinduzi 2024 wakiwa kwenye ardhi ya Bongo.
Katika mechi nne ambazo walicheza safu ya ushambuliaji ya Yanga ilifunga jumla ya mabao 8 huku ukuta wao uliokuwa na Gift Fred uliokota mabao manne kibindoni.
Ali Kamwe, Ofisa Habari wa Yanga ameweka wazi kuwa kumaliza mwendo kwenye Mapinduzi 2024 hawajakata tamaa ya kuendelea na mapambano wapo imara.
“Kupoteza kwenye Mapinduzi sio mwisho wa kila kitu bado tupo na tutafanyia maboresho yale yaliyotokea kwa ajili ya kupata matokeo kwenye mashindano mengine.
“Mpira una matokeo yake ambapo yupo anayeshinda na yule ambaye anashindwa hivyo hakuna sababu ya kuendelea kufikiria sana kwa yale yaliyotokea ambacho tunaangalia kwa sasa ni wakati wetu ujao,” amesema Kamwe.