IMEELEZWA kuwa Simba muda wowote watakamilisha usajili wa mshambuliaji wa Klabu ya Comerciantes FC, Mauricio Cortes raia wa Colombia.
Simba imepanga kukifanyia maboresho makubwa kikosi chao, kati ya hayo ni safu ya ushambuliaji ambayo Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha amependekeza usajili huo.
Safu hiyo ya ushambuliaji hivi sasa inaongozwa na John Bocco, Jean Baleke, Kibu Denis na Moses Phiri ambaye yeye huenda akasepa katika timu hiyo, mwishoni mwa msimu huu.
Mmoja wa mabosi wa Simba ameliambia Championi Ijumaa kuwa, wapo katika hatua za mwisho za kumsajili mshambuliaji huyo ambaye ana uwezo kucheza kama winga akitumia mguu wa kushoto.
Bosi huyo alisema kuwa, kabla ya kufikia makubaliano hayo na mshambuliaji huyo, walimfuatilia kwa karibu kujua uwezo wake wa kufunga na kutengeneza nafasi za mabao.
Aliongeza kuwa mshambuliaji huyo hivi sasa anakamilisha taratibu zake za uhamisho ambaye atasaini mkataba wa miaka miwili ya kuichezea Simba ambayo inashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Katika kipindi cha dirisha dogo ngumu kumpata mchezaji ambaye hana mkataba, lakini tumempata Cortes tuliyefikia makubaliano mazuri ya kusaini mkataba wa miaka miwili.
“Cortes tutamtumia katika mashindano ya kimataifa ambayo tunashiriki, kutokana na kutocheza Ligi ya Mabingwa Afrika ambayo hivi sasa ipo katika hatua ya makundi.
“Ujio wake kutamuondoa mchezaji mmoja wa kigeni kati ya hawa waliokuwepo katika timu, na kocha ndiye atakayetoa mapendekezo ya nani wa kuachwa katika dirisha dogo,” alisema bosi huyo.
Akizungumzia usajili huo, Meneja wa Habari wa timu hiyo, Ahmed Ally alisema: “Jukumu la usajili lote tumemuachia kocha ambaye yeye ndiye atakayependekeza mchezaji wa kuachwa na kusajiliwa, kikubwa hatutaki kumuingilia kocha wetu.”