BEKI wa zamani wa Manchester United, Gary Neville, amesema Arsenal ndiyo timu pekee inayoweza kutoa ushindani kwa Manchester City katika kuwania ubingwa wa Premier League msimu huu.
Kauli ya Muingereza huyo imekuja kufuatia Liverpool kushindwa kuifunga Manchester Utd katika mchezo wa Premier uliochezwa Anfield, juzi Jumapili.
Arsenal wamerejea kileleni mwa msimamo wa Premier, baada ya kuifunga Brighton mabao 2-0, na kuishusha Liverpool hadi nafasi ya pili, wakati Aston Villa ikiwa ya tatu, Man City inakamata nafasi ya nne.
“Sidhani kama Arsenal ni timu pekee itakayotoa ushindani kwa Man City, awali kabla ya Liverpool kutoka suluhu na Man United, niliona ushindani ni mkubwa, lakini imetokea hivi, lakini kama Arsenal itaimarika zaidi na kutopata majeraha kama msimu uliopita, ninaamini watakuwa na timu bora zaidi ya kushindania ubingwa,” alisema Neville.
Wakati huohuo, Neville ameitetea Man City kutokana na siku za karibuni kutokuwa kwenye kiwango bora baada ya kushinda mechi moja pekee ya Premier League kati ya sita.
“Hii siyo Man City tunayoifahamu, ninaamini kuna upepo mbaya umewatembelea, watu wasiiseme vibaya, kama wakiendelea kuwa pale walipo hadi kufikia Februari, basi watakuja kuwa tishio zaidi,” alibainisha Neville