BENCHIKHA AANZA MASHINE NNE SIMBA SC

RASMI Kocha Mkuu wa Simba raia wa Algeria, Abdelhak Benchikha ameikabidhi Bodi ya Wakurugenzi ya klabu hiyo, majina ya wachezaji wanne anaotaka wasajiliwe katika dirisha dogo la usajili msimu huu.

Hiyo ni katika kuhakikisha anatengeneza kikosi imara kitakacholeta ushindani katika msimu huu ambao wamepanga kufika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Wapo baadhi ya wachezaji wanaohusishwa kujiunga na Simba katika dirisha hili dogo, baadhi ni beki wa kati wa Coastal Union, Lameck Lawi na kiungo wa Mtibwa Sugar, Ladack Chasambi.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, Benchikha amekabidhi ripoti ya usajili baada ya kukaa wiki moja na nusu na kikosi hicho tangu akabidhiwe timu hiyo.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa katika ripoti hiyo aliyoikabidhi, ameonekana kuhitaji mshambuliaji mmoja wa kati mwenye uwezo wa kufunga na kutengeneza naafasi za mabao kwa wachezaji wenzake.

Aliongeza kuwa pia anahitaji kiungo, winga na beki wa kushoto atakayesaidiana na Hussein Mohammed ‘Tshabalala’ ambaye yupo pekee katika anayemudu kucheza nafasi hiyo.

“Simba imepanga kufanya maboresho makubwa katika baadhi ya nafasi, ni baada ya Benchikha kukabidhi ripoti ya usajili ambayo inahitaji wachezaji zaaidi ya wachezaji katika usajili huu wa dirisha dogo.

“Tayari uongozi umemuhakikisha fungu la fedha la kutosha likalokamilisha usajili wa wachezaji ambao yeye mwenyewe amewapendekeza katika usajili huu wa dirisha dogo unaofunguliwa kesho (leo Ijumaa).

“Kocha ameachiwa jukumu lote la usajili, kwa wale wachezaji anaowataka ambao anaamini watakiboresha kikosi chake, kati ya hao wapo wa kigeni ambao baadhi alifanya nao kazi na klabu alizopita,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mtendaji (C.E.O) wa Simba, Imani Kajula hivi karibu alizungummzia hilo la usajili kwa kusema kuwa: “Masuala yote ya usajili, tumemuachia kocha wetu ambaye anaamua wachezaji wa kusajiliwa na kuachwa, hivyo hatutamuingilia katika hilo.”

NA WILBERT MOLANDI, CHAMPIONI IJUMAA