MWENDO WAO KIMATAIFA HALI NI MBAYA KWA WAWAKILISHI WETU

WIKI chache nyuma lilikuwa ni gumzo la kuanza kwa Ligi ya Mabingwa Afrika katika hatua ya makundi na Tanzania ilikuwa kati ya nchi chache kabvisa zenye timu mbili katika hatua hiyo.

Simba na Yanga wote walipata nafasi ya kuingia kwenye hatua hiyo ya makundi, hatua ambayo sote tunafahamu timu bora tu ndizo hufanikiwa kufika hapo.

Kwa timu nyingi sana kufikia hatua hiyo halijawahi kuwa jambo dogo na anayefikia hatua hiyo hajawahi kuonekana mwepesi.

Mfano kwa nyumbani Tanzania, Simba wamekuwa ni timu ambayo inaingia katika hatua hiyo mara kwa mara na unaona ndanio ya misimu saba wanaweza kuwa wamepata nafasi hiyo mara nne au tano.

Kwa watani wao Yanga ambao msimu uliopita waliamka kimataifa na kuishangaza Afrika kwa kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho na bado hawakupoteza kinyonge, hawajawahi kushiriki hatua ya makundi tokea mwaka 1998.

Wakati wameingia, baada ya mechi mbili walizocheza wamefanikiwa kupata pointi moja tu baada aya sare ya juzi dhidi ya Al Ahly, huku wakiwa wamepokea kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria.

Maana yake, tokea 1998, hadi leo bado Yanga hawajafanikiwa kushinda mchezo wowote wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ukirejea kwa watani wao ambao ni wazoefu, kwani hata msimu uliopita walikuwa katika hatua hiyo, msimu huu ni mgumu kwao pia.

Hawajapoteza, lakini wamepata sare mbili, nyumbani Dar es Salaam dhidi ya Asec lakini hata ugenini dhidi ya Jwaneng ya Botswana.

Katika kundi lake, Yanga wanaburuza mkia baada ya Ahly, Belouizdad, Medeama ya Ghana na katika kundi lake Simba pia wanakaribia mkiani pia maana wako nafasi ya tatu baada ya Asec, Jwaneng na mbaya zaidi kigogo Wydad ndio wanaoburuza mkia.

Kwa Wydad kuwa mkiani maana yake mechi ijayo ya Simba ugenini pale Marrakech, Morocco itakuwa ngumu sana na kama Simba hatapa pointi, kucheza mechi tatu uwe na pointi mbili, si jambo zuri na ni dalili za ugumu wa kutoka hapo ulipo.

Wydad atakuwa anafanya kazi ya ziada kuondoka alipo na kuingia katika nafasi zile mbili, sasa analazimika kuzipigania sana kwa kuwa awali alionekana ndiye alipaswa kuwa wa kwanza kwenye hatua ya mtoano.

Simba wanapaswa kujipanga sana na bahati mbaya mechi zimefuatana na wao watalazimika kusafiri safari ndefu baada ya ile ndefu ya Botswana na Wydad watakuwa wakiwasubiri. Bila shaka, wameanza na mguu mbaya na wana kazi ngumu sana kurekebisha maana mechi zilizobaki ni nne tun a katika tatu za nyumbani, tayari moja Simba ‘wameichezea’.

Kwa Yanga pia mguu ni mbaya vilevile, maana mechi mbili pointi moja lakini aliyekuwa kibonde wa kundi Medeama baada ya kuanza na kipigo ugenini Misri ameibuka na kumtwanga Belouizdad alipowatembelea kwao Ghana. Hii maana yake Cairo patakuwa pagumu, Kotoko hali kadhalika na mechi mbili za nyumbani dhidi ya Belouizdad na Medeama zinatakiwa pointi sita zibaki ili kurejesha uhai.

Kuna kila sababu ya timu zetu hizi mbili, kila mmoja kwa upande wake aka echini na kujipanga vilivyo kwa kuwa litakuwa jambo kubwa zaidi kama zitafuka hatua hii lakini litakuwa jambo la aibu sana pia kama tutakosa hata timu moja kwenda hatua inayofuata.

Inawezekana kabisa kama maandalizi yatakuwa ni ya kutosha kwa mechi mbili zijazo kwanza kuhakikisha kila timu inachota pointi.

Najua, Yanga malengo yao ilikuwa ni kufika makundi na wamefanikiwa. Lakini ikiwezekana wakaenda na mwendo kama wa msimu uliopita kuongeza lengo kila wanapopiga hatua.

Simba anataka kuvuka robo fainali ambayo imekuwa ni kama mwisho wao lakini sasa hawawezi kufanya lolote hadi watoke makundi na wao ni wazoefu, wanalijua hilo na sasa wana kocha mpya hivyo tuamine wanaweza kubadilisha mambo.